Monday, June 20, 2011

CHILUBA HATUNAE TENA



“Daktari alifika nyumbani na kumpa matibabu na kupata nafuu, lakini baadaye alipoteza fahamu,” alisema Mwamba.Aliongeza kuwa Chiluba alifariki nyumbani kwake saa 6 usiku akiwa amezungukwa na mke wake na ndugu zake wengine. 

Kwa muda mrefu Chiluba amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo tangu alipoondoka madarakani na mara kadhaa amekuwa akipatiwa matibabu nje ya nchi.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 1991, Chiluba alionekana ‘Mkombozi’ baada ya miaka 27 ya utawala wa Kijamaa wa chama kimoja chini ya Rais wa kwanza wa Zambia, Dk Kenneth Kaunda.

Licha ya kusifiwa kwa kuinua uchumi wa Zambia katika kipindi cha utawala wake, baada ya kuondoka makarakani aliandamwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma na kufumbia macho vitendo vya ufisadi.
Chini ya utawala wa Chiluba, Zambia ilichukuliwa kuwa ni nchi ya mfano katika Demokrasia ya Afrika na utawala wake ulikuwa ukiungwa mkono na nchi za Magharibi.

Hata hivyo baada ya kuondoka madarakani, aliandamwa na tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa, kutumia vibaya madaraka, kukandamiza wapinzani, kufukuza watu kazi na kuwafunga jela waandishi wa habari.
Mwishoni mwa kipindi cha uongozi wake, alijaribu kubadilisha Katiba ya nchi hiyo ili imruhusu kugombea kipindi cha tatu, lakini alishindwa kutokana na wananchi kuandamana kupinga jambo hilo.
Mwaka mmoja tangu atoke madarakani alishtakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka, lakini aliachiwa huru na mwaka 2007, alitiwa hatiani na mahakama moja mjini London, Uingereza kwa udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za umma na kuamriwa kulipa Dola za Marekani 58 milioni. 
Hata hivyo, uamuzi wa hukumu hiyo haukutekelezwa.
Historia yake
Chiluba aliingia madarakani akiwa Rais wa pili wa Zambia baada ya kumshinda Dk Kaunda katika uchaguzi wa kwanza uliyoshirikisha vyama vingi nchini Zambia.

Chiluba alikuwa ni mfuasi wa Kaunda wakati wa mapambano ya kupigania uhuru mwaka 1964, lakini alikuja kuasi baada ya Zambia kuingia katika mfumo wa chama kimoja.

Mwaka 1980, Chiluba alitishia kuitisha mgomo wa nchi nzima kupinga utawala wa Kaunda.
Baada ya miezi kadhaa ya ghasia za kupinga utawala wa Kaunda, Chiluba na viongozi wengine wa vyama vya wafanyakazi nchini humo, walikamatwa na kuwekwa kizuizini hadi mahakama ilipoamuru waachiwe baada ya kuonekana walishikiliwa kinyume cha sheria.

Baada ya kuachiwa, Chiluba alinzisha Chama cha Movement for Multi-Party Democracy (MMD) mwaka 1990 na kuwa chama pinzani dhidi ya United National Independence Party (UNIP) cha Dk Kaunda.
Kufuatia nchi hiyo kukabiliwa na hali mbaya ya uchumi, ukosefu wa ajira, madeni ya nje na mfumuko wa bei, Chiluba alishinda katika uchaguzi wa mwaka 1991 kwa kupata zaidi ya asilimia 80 na kuwa rais wa Zambia hadi mwaka 2001.

Shutuma za rushwa
Mwaka mmoja baada ya kuachia madaraka, Zambia ikiongozwa na marehemu Levy Mwanawasa, alifunguliwa zaidi ya mashtaka 100 ya rushwa ikiwamo tuhuma za wizi wa Dola za Marekani 35 milioni, fedha za umma, ambazo inadaiwa alificha nje ya nchi.
Mke wake, Regina Chiluba, pia alishtakiwa kwa tuhuma za wizi wa fedha za umma na rushwa, mashtaka ambayo aliyakana akidai kuwa yalikuwa na mwelekeo wa kisiasa.

Mahakama ilifuta kesi hiyo ya Regina baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kuwa alitumia mgongo wa mume wake kutumia vibaya fedha za umma.

Hata hivyo, mwaka 2009, Regina alihukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kupokea fedha za umma zilizoibwa na kununua nyumba tatu za kifahari mume wake akiwa madarakani.

No comments:

Post a Comment

Tunayaheshimu maoni yako ndio maana tunayahitaji