Tuesday, July 19, 2011

Bajeti ya Nishati yatupiliwa mbali na  Serikali ya JK
Waziri Ngereja

WAKATI Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akijipanga kujibu hoja za wabunge kesho, bajeti yake ipo hatarini kukwamishwa kutokana na wabunge wengi kuonyesha msimamo wa kutoiunga mkono.

Miongoni mwa mambo ambayo yanaifanya bajeti hiyo ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa mwaka 2011/12 kuwekewa vikwazo ni tatizo la umeme ambalo linalikumba taifa kwa sasa, uwiano usio sawa katika miradi ya usambazaji wa nishati hiyo na mikataba mibovu katika sekta ya madini na nishati.

Tayari, wabunge wengi wakiwamo wa CCM wametoa misimamo mikali dhidi ya bajeti hiyo na tofauti na wizara nyingine ambazo zilipingwa na wabunge wa upinzani pekee.

Miongoni mwa kauli kali zilizotamkwa na wabunge na hata kuwashangaza wengi ni kama vile, "Hapa patachimbika!" "Nitawaunga mkono wapinzani kuwa Serikali hii ni legelege".

Nyingine ni, "Waziri amesema uongo", "Waziri anapendelea miradi katika majimbo ya maswahiba wake" na "Siungi mkono hoja."

Ingawa wabunge wa CCM, Alhamisi usiku  walifanya kikao chao cha kamati ya chama kuweka mkakati wa kutoipinga, lakini hali inaonyesha kuwa tofauti kabisa.

Kitu kingine ambacho kinaashiria hali itakuwa mbaya kwa waziri huyo ni uamuzi wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini chini ya January Makamba kuonyesha wazi kuwa haiiungi mkono bajeti hiyo, tofuati na kamati zingine za wizara zilizopita ambazo zilikosoa, lakini kwa lugha laini.

Mwenyekiti wake, Makamba alimshambulia waziwazi Ngeleja akisema  tatizo la umeme usio wa uhakika limedumu kwa muda mrefu na sasa limekuwa janga.

"Janga hili limeleta adha kwa wananchi, limeleta athari kubwa kwa uchumi, na fedheha kwa nchi na kwa Serikali," alilalamika Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli.

Alisema kwa miaka mingi sasa Serikali imekuwa ikisema inafanya juhudi za kutatua tatizo, lakini hazijazaa matunda kwani tatizo limeendelea kuzidi.

Makamba ambaye kwa miaka mitano alikuwa msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete akiwa Ikulu, alisema kamati yake inakubali kwamba upungufu wa mvua umeendelea kuathiri uzalishaji wa umeme kwa sababu kwa kiwango kikubwa nchi yetu inategemea umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji yanayotokana na mvua.

Hata hivyo, akasema kamati inaamini kwamba sababu hii ya upungufu wa mvua haiwezi kuendelea kuwa sababu kwani mwenendo wa mvua na majira ya mvua yanajulikana kwa miaka mingi sasa.

Makamba ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba alisema Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo karibu vyote vya kuzalisha umeme kama vile, gesi asilia, jua, upepo na makaa ya mawe.

Kama hiyo haitoshi, Ngeleja aliendelea kuonjeshwa shubiri na wabunge mbalimbali wa kutoka katika chama chake, CCM.

Miongoni mwa wabunge hao wa CCM waliotemea cheche kuhusu bajeti ya Nishati na Madini ni pamoja na Nimrod Mkono (Musoma Vijijini), James Lembeli (Kahama), Charles Mwijage (Muleba Kaskazini), Anne Kilango Malecela (Same Mashariki) na Ally Mohamed (Nkasi Kaskazini).

Mkono alimshangaa Ngeleja akisema katika hotuba yake kwamba mgodi wa Buhemba kwa sasa uko chini ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na wanatafuta mbia.

Alisema ukweli ni kwamba Ngeleja hakujua alichokuwa anakisema kwa sababu mali na zana zote zilizokuwa kwenye mgodi huo zimeibiwa na umebaki mtupu.

Kwa sababu hiyo, akamtaka Ngeleja aliambie Bunge mtu aliyehusika na wizi huo vinginevyo hataunga mkono bajeti yake.

Alipendekeza kuwa badala ya kuweka walinzi kulinda mgodi huo ambao hauna kitu ndani yake, wapatiwe wachimbaji wadogo wadogo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinyanyasika kwa kukosa maeneo.

Lembeli, yeye kwa upande wake alilalamikia wakazi wa jimboni kwake kuwa wamekuwa maskini katika nyanja zote zikiwamo afya, elimu, uchumi na miundombinu wakati wageni kutoka nje ya nchi wakifaidika kwa madini wanayochimba eneo hilo.

Alilalamika kuwa wanachoambulia wananchi wake ni mauaji na dhuluma, hivyo akasisitiza: "Mimi siungi mkono hoja hadi haya ninayozungumza yakipatiwa ufumbuzi."

Mwijage alisema kama Serikali ingeweza kuongeza Sh10 ya kodi kwa kila lita ya mafuta, kwa mwaka mmoja yangepatikana mabilioni ya fedha ambayo yangetatua tatizo la umeme.

Lakini, akaishauri Serikali kutumia nyongeza ya kodi ya Sh400 iliyoongeza kwa kila lita ya mafuta ya taa kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya umeme.

Kilango, kwa upande wake akitumia lugha kali alimtupia shutuma, Waziri Ngeleja akisema uwekezaji wa miradi ya umeme umependelea zaidi baadhi ya mawaziri wakati kwenye jimbo lake akilaghaiwa.

Alitaja baadhi ya mawaziri waliopendelewa kuwa ni Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) wa Jimbo la Same Magharibi, Aggrey Mwanri  (Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- Tamisemi) kutoka Jimbo la Siha na Profesa Jumanne Magembe (Kilimo, Chakula na Ushirika) ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga.

Kilango alilalamika pia kwamba kwenye hotuba ya Ngeleja alitaja vijiji ambavyo vimesambaziwa umeme huo kwenye jimbo la Same Mashariki, lakini ukweli vyote vipo Same Magharibi, kwa Dk Mathayo.

Hakutaja vijiji hivyo, lakini kwa mujibu wa hotuba ya Ngeleja vijiji hivyo ni Mhezi, Ijinyu, Kijom, Msindo, Mbakweni, Kizungo na Digo.

Hivyo, alimtaka Waziri Ngeleja kuacha kudanganya Watanzania na huku akionyesha upendeleo wa wazi kwa kupeleka miradi mingi ya umeme kwenye majimbo ya maswahiba wake.

Kilango alisema; "Sisi (wabunge) wote tuko hapa kwa kazi moja tu nayo ni (kujadili) kuondoa matatizo ya Watanzania. Lakini, mengine tunayoyafanya ni ya kitoto."

Akionyesha kukasirishwa na kuzungumza kwa jazba.mbunge huyo alisema tatizo la umeme linawatesa sana Watanzania.

Akaitaka Serikali iachane na mpango wa kufikiria yenyewe namna ya kutatua tatizo la umeme nchini na badala yake iwashirikishe na wengine.

Mbunge mwingine ni Ally Mohamed ambaye alimlaumu Ngeleja kwa kile alichosema ni kudanganya kwenye hotuba yake kuwa katika wilaya ya Nkasi, tayari mradi wa kusambaza umeme umetekelezwa kwa asilimia 62.

Mohamed alisema mara baada ya Ngeleja kumaliza hotuba yake na kuomba kutoa taarifa kuwa waziri huyo amedanganya.

"Alisema njia ya umeme wa msongo mkubwa umekamilika na usimikaji wa nguzo umetekelezwa kwa asilimia 62. Huu ni uongo. Hakuna hata nguzo iliyochimbiwa," alilalamika Mohamed.

Alisisitiza kwamba hataunga mkono hoja ya waziri huyo kijana kwa sababu kuna udanganyifu na kuonya kwamba kama ni maofisa wake, basi walimpelekea taarifa potofu.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Hai-Chadema) aliliambia Bunge juzi kuwa uhaba wa umeme unaolikumba taifa kwa sasa linatokana na tatizo la uongozi.

"Hakuna 'seriousness' (umakini) katika kutatua tatizo la umeme," alisema Mbowe wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Alisema kuwa tatizo la umeme limekuwa likilikabili taifa kutokana na Serikali kutekeleza mipango yake kisiasa.

Alielezea miradi mingi iliyopo kwenye bajeti inatokana na taarifa za kusikia kuhusu wafanyabiashara ambao wanahisia za kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini.

Na hilo, akasema ndilo linalosababisha mara nyingi miradi mingi kuonekana kwenye makaratasi, lakini utekelezaji wake haupo.

Alionya kuwa tatizo hilo limekuwa likionekana ni dogo, lakini linawaathiri watu wengi, hasa kampuni na viwanda vilivyowekezwa nchini na linavitishia kuviangamiza kabisa.

Hali inavyonekana kwa sasa, alisema inaashiria kuwa Waziri Ngeleja amezidiwa kutokana na kurundikiwa mambo mengi ayafanye kwa wakati mmoja.

Kwa sababu hiyo, Mbowe akapendekeza wizara hiyo igawanywe mara mbili kutokana na unyeti wa mambo iliyo nayo juu ya sekta ya madini na nishati.

Hata hivyo, aliwafurahisha baadhi ya wabunge alipoeleza kushangazwa na kitendo cha Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kutoa shutuma kali dhidi ya wizara, akisema alitegemea cheche za namna hiyo kutolewa na vyama vya upinzani, hivyo akamtaka mwenyekiti wa kamati hiyo, January Makamba kuihama CCM na kujiunga Chadema ili aweze kutumia vizuri mawazo hayo.

Hata hivyo, baada ya kumaliza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alitoa taarifa kuwa kamati ya Makamba ina wajibu wa kuikosoa Serikali.

Alisema kamati ile inajumuisha wabunge wa pande zote, hivyo si ya CCM na ina wajibu wa kuikosoa na kuishauri Serikali.


Nayo Kambi ya Upinzani Bungeni imesema kuwa tatizo sugu la mgawo wa umeme limekuwa sugu na kutaka serikali ilitangaze kuwa ni janga la taifa ambalo limetokana na ufisadi na udhaifu wa kiuongozi na kiutendaji ambao umeikabili sekta ya nishati nchini kuanzia awamu ya pili.

Kambi hiyo ilitoa kauli hiyo kupitia msemaji wake kuhusu Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika (Ubungo-Chadema), wakati akichangia hotuba ya bajeti iliyosomwa na Waziri Ngeleja.

Mbali na kulitangaza kuwa janga la kitaifa, Mnyika alitaka viongozi waliohusika kuwajibishwa na iundwe kamati kulichunguza kwa undani jambo hilo, vinginevyo kambi ya upinzani itahamasisha maandamano nchi nzima.

Alitaja madhara mengine ya kifisadi ni hasara ya mchakato wa ubinafsishaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), uzembe wa Net Group Solution, ufisadi wa Kiwira, kashfa ya Alstorm Power Rentals, sakata la Songas/Pan African Energy na ufisadi wa Richmond.

Madhara mengine aliyataja kuwa ni yale yaliyotokana na Dowans ambayo sasa mitambo yake iko chini ya Symbion.

Alisema pamoja na uamuzi ya Bunge la tisa ya kuhusu masuala hayo bado kambi ya upinzani inataka hatua kamili kuchukuliwa kwa wahusika wa kashfa hizo kama walivyotajwa kwenye orodha ya mafisadi ili kujenga msingi wa kuepusha hali kama hiyo kujirudia katika uwekezaji unaondelea hivi sasa.


Hata hivyo, awali akisoma bajeti ya wizara hiyo, Ngeleja alitaja miradi ipatayo 16 ambayo Serikali imekusudia kuitumia ili kutatua tatizo la umeme moja kwa moja.

Ngeleja alisema kuwa mpango wa bajeti hiyo umezingatia mikakati mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa kama vile, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano, Malengo ya Maendeleo ya Milenia na sera za CCM.

"Lengo la Serikali ni kuimarisha na kuboresha sekta ya nishati na kuongeza fungamanisho la sekta ya madini na sekta nyingine," alisema Ngeleja.

Miongoni mwa miradi aliyoitaja Ngeleja ni mradi wa mitambo ya kufua umeme ya megawati 100 ulioko Ubungo jijini Dar es Salaam ambao utakamilika Desemba mwaka huu na megawati 60 jijini Mwanza ambao utakamilika Juni mwakani.



SOURCE: http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/40-habari-mwananchi-jumapili/13728-bajeti-ya-nishati-moto-kwa-serikali-ya-jk.html

No comments:

Post a Comment

Tunayaheshimu maoni yako ndio maana tunayahitaji