Thursday, August 25, 2011




Hazina yatakiwa kuharakisha fedha za 


wazee EAC








WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ameiomba Wizara ya Fedha kuharakisha kuwalipa Wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wenye madai halali kwa kuwa suala hilo linaharibu sura ya nchi kwenye jumuiya hiyo.

Sitta aliyasema hayo jana wakati akitoa majumuisho ya hoja za Wabunge walizozitoa wakati wakichangia bajeti yake ya mwaka 2011/2012 aliyoiwasilisha Bungeni juzi. Hata hivyo Bunge lilipitisha bajeti hiyo ya Sh bilioni 16.4.
Alisema ni vyema Hazina wakaharakisha kukokotoa majina ya wadai halisi na kuwatoa hofu wadai hao kwa kuwa wengi wao walifanya kazi katika utaratibu wa vibarua.
“Ni kweli sasa ni mwaka wa 34, bado hawajalipwa ila kazi inaendelea, naiomba Wizara ya Fedha kuharakisha jambo hilo, kweli ni tatizo na tatizo lenyewe linatokana na ukweli kwamba wengi walifanya kazi kama vibarua,” alisema Sitta akifanya majumuisho ya hoja za wabunge.
Katika hatua nyingine, Sitta alisema kutokana na Jumuiya hiyo bado kufahamika sawasawa na Watanzania, hakutakuwapo na kuharakisha tena kwa Shirikisho, bali kwenda hatua kwa hatua ili nchi ijiridhishe.

No comments:

Post a Comment

Tunayaheshimu maoni yako ndio maana tunayahitaji